NASA watoa matokeo ya kura za urais, Agosti 8

Muungano wa NASA umetoa matokeo yake ya uchaguzi wa urais kwa uchaguzi mkuu uliokumbwa na utata wa Agosi 8 mwaka wa 2017, siku moja kabla ya hafla ya kuapishwa kwa Raila Odinga na Kalonzo Musyoka kama Rais na naibu wa rais wa wananchi katika kaunti ya Homa Bay hapo kesho. Kulingana na matokeo yaliyotolewa na kiongozi wa timu ya wanasheria ya NASA ambaye pia ni Seneta wa Siaya James Orengo, Raila Odinga alishinda uchaguzi huo kwa kura 8,104,744 zilizowakilisha asilimia 50.24 dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta ambaye alipata kura 7,908, 215 zilizowakilisha asilimia 48.92 ya kura zote. Mbunge mteule wa chama cha ANC, Godfrey Osotsi, alidai kwamba taarifa waliyopokea kutoka kwa sava ni ya kuaminika. Osotsi ambaye pia ni mtaalamu wa teknolojia ya mawasiliani ya habari, IT, alisema muundo mbinu waA�A�IEBC ulivurugwa na wavamizi wa kimtandao ambao walibadili matokeo hayo ili kumpendelea Rais Uhuru Kenyatta. Kulingana na matokeo yaliyotangazwa na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, Rais Kenyatta alishinda uchaguzi wa Agosti 8 kwa kura 8,203,290 dhidi ya kura 6,762,224 alizopata Raila Odinga.