NASA wamsifia Nkaissery kama mzalendo

Muungano wa NASA umeungana na wakenya na hasa jamii ya wamaasai katika kutuma risala za rambi rambi kwa jamaa , ndugu na marafiki wa marehemu aliyekuwa waziri wa usalama wa kitaifa Joseph Nkaisseiry. Wakiwahutubia wanahabari mjini Mombasa, mwaniaji urais wa muungano huo Raila Odinga na mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka walimwelezea Nkaissery kuwa mzalendo aliyejitolea kuhakikisha usalama wa nchi hii alipokuwa akihudumu kama mwanajeshi na kama waziri wa usalama wa kitaifa. Raila amesema Nkaissery aliwakilisha nchi hii katika makongamano mbali mbali ya kimataifa katika kushughulikia changamoto za kiusalama. Wakati huo huo Raila ameondolea mbali hofu kuwa kutatokea ghasia baada ya uchaguzi mkuu ujao katika baadhi ya sehemu za nchi.

Kwa upande wake Kalonzo amekiri kuwa licha ya kushikilia misimamo mbali mbali ya kisiasa hasa wakati wa kampeni za Okoa Kenya upinzani ungali unatambua kuwa Nkaissery alikuwa tu akitekeleza majukumu yake rasmi ya kiserikali. Amesema jamii ya wamaasai katika siku za hivi majuzi imepoteza viongozi kadhaa akiwemo Prof. George Saitoti, William Ole Ntimama na John Keen.