NASA kumwapisha Raila iwapo hakutakuwa na mazungumzo

Kiongozi wa walio wachache katika bunge la taifa, John Mbadi na mwenzake wa bunge la Seneti, Moses Wetangula, wamesema kwamba mipango ya kumwapisha kiongozi wa muungano wa NASA Raila Odinga mwisho wa mwezi huu itaondolewa ikiwa serikali itaanza mpango wa kushauriana na upinzani. Walisema upinzani uko tayari kusimamisha mipango hiyo ikiwa maswala muhimu yatajadiliwa miongoni mwao marekebisho ya taratibu za uchaguzi. Viongizi hao waliokuwa wakizungumza wakati wa mkutano na balozi wa Marekani hapa nchini, Robert Godec, walisema nchi hii inastahiki wakenya wote kwenda mbele na wala sio baadhi ya wananchi.

Balozi Godec amekuwa mstari wa mbele kuitisha mazungumzo kati ya makundi mawili makuu ya kisiasa hapa nchini akisema kwamba nchi hii inahitaji kusonga mbele baada ya kipindi kirefu cha uchaguzi. Balozi huyo wa Marekani aliongeza kwamba ipo haja ya kuwepo kwa utaratibu wa mazungumzo kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Raila ili kuisaidia nchi hii kuzingatia maswala mengine ya maendeleo. AwaliA�A�Rais Kenyatta alidumisha kwamba ataweza kukaa kwenye meza ya mazungumzo kuhusu maendeleo lakini sio siasa.