Naibu Rais,Ruto ahakikishia wakaazi wa Kerio Valley usalama wa mifugo yao

Naibu wa Rais, William Ruto, amewahakikishia wakazi wa eneo la Kerio Valley kuwa serikali itakomesha wizi wa mifugo katika sehemu hiyo. Akiongea kwenye maadhimisho ya tano ya utamaduni na mnada wa mbuzi wa Kimalel katika kaunti ya Baringo Ruto aliwataka viongozi katika eneo la Kerio Valley kuwa wakakamavu na kushirikiana katika kukabiliana na wizi wa mifugo. Ruto alisema wizi wa mifugo na utamaduni uliopitwa na wakati na haufai kuendelezwa huku wananchi katika maeneo mengine ya nchi wakishiriki katika shughuli za kuwaletea mapato na kuboresha maisha yao. Naibu wa Rais alisema viongozi kutoka kaunti za Turkana, Baringo, Elgeyo Marakwet, Samburu na Pokot Magharibi sharti washirikiane kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika kupata suluhu ya la kudumu kwa tatizo hilo. Alisema ni haki ya Wakenya wote kuishi kwa amani na kwamba wale wachache wanaovunja sheria watachukuliwa hatua. Viongozi hao waliahidi kuwa watakutana na kubuni mikakati ya kuhakikisha amani na uthabiti katika eneo hilo. Seneta wa Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen alisema kuna mipango ya viongozi kukutana na kubuni njia za kumaliza wizi wa mifugo kwenye eneo hilo.