Naibu Rais William Ruto Kuhutubia Wajumbe Wa Jubilee

Naibu wa Rais William Ruto leo alasiri atahutubia maelfu ya wajumbe kutoka vyama 11 tanzu vya uliokuwa muungano wa Jubilee waliokongamana katika uwanja wa Karasani kuidhinisha kubuniwa kwa chama kimoja cha jubilee. Hafla ya leo inatangulia mkutano mkubwa wa kesho ambapo rais Uhuru Kenyatta atazindua rasmi chama kipya cha Jubilee. Rais Kenyatta vile vile anatarajiwa kuwatangaza wanachama wa baraza kuu la kitaifa la chama hicho.

Wakati huo huo,A�Wajumbe wa chama cha Jubilee wamemiminika kwenye uwanja wa michezo wa Kasarani kwa mkutano wa wajumbe ambapo wanatarajiwa kuidhinisha katiba na nembo ya chama hicho kipya. Rais Kenyatta anatarajiwa kuteuliwa kuwa kaimu kiongozi wa chama hicho huku naibu wake, William Ruto akiteuliwa naibu kiongozi wa chama hicho. Viongozi wanaohudhuria mkutano huo wamesema chama hicho kitawaunganisha wakenya wote. Akiongea na shirika la utangazaji nchini KBC, gavana wa Bungoma Kenneth Lusaka alisema chama kipya cha jubilee kitakachozinduliwa rasmi hapo kesho kina sura ya kitaifa. Matamshi yake yaliungwa mkono na naibu spika wa bunge la kitaifa Joyce Laboso. Lusaka alipuzilia mbali madai ya kuwepo kwa migawanyiko kwenye chama cha New Ford Kenya ambacho sasa kimevunjwa akisema anaungwa mkono na wafuasi wake kujiunga na Jubilee.