Naibu Rais William Ruto Asema Serikali Iko Tayari Kwa Mazungumzo Na Upinzani Kuhusu Uchaguzi

Naibu wa Rais William Ruto amesema serikali iko tayari kuuhusisha upinzani katika mazungumzo ya kutatua swala lolote kabla ya uchaguzi mkuu mwaka ujao. Alisema serikali itazingatia katiba kutatua swala lolote ikiwemo hatima ya tume huru ya uchaguzi na mipaka Nchini (IEBC). Hata hivyo alisema upinzani hauwezi kutumia maandamano na vitisho kuilazimisha serikali.

Ruto alisema wabunge wanapaswa kufanya mazungumzo yatakayojumuisha maoni kutoka kwa viongozi wa kidini, makundi ya kijamii, wataalamu na wakenya wengine. Akizungumza wakati wa ibada ya wafu kwa Lucia Njoki Mungai katika kijiji cha Kamuguri eneo bunge la Gatundu Kusini kaunti ya Kiambu Naibu wa Rais alisema hakuna anayeweza kuondolewa ofisini kupitia maandamano.A�

Alisema hayo huku wabunge wa muungano wa Jubilee wakiwaomba viongozi wa muungano wa CORD wakomeshe vitisho kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Walisema upinzani unatumia njia ambazo sio halali kama mkakati wa kuilazimisha serikali kufanya mazungumzo kuhusu hatima ya tume hiyo ya uchaguzi. Waziri wa Ugatuzi Mwangi Kiunjuri na Gavana wa kaunti ya Bungoma Ken Lusaka walisema serikali haiogopi upinzani kwa sababu inafuata utaratibu ufaao kutimiza ahadi ilizotoa.