Naibu Rais William Ruto Aahidi Wakenya Kutatuliwa Kwa Matatizo Ya IEBC

Naibu Rais William Ruto amewahakikishia wakenya kwamba maswala machache tata yaliyosalia kuhusiana na tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) yatatatuliwa hivi karibuni ili kufanikisha mashauriano. Ruto alisema ana imani kuwa maswala hayo yaliyosalia ambayo yaliibuliwa na pande husika yatasuluhishwa katika muda wa siku chache zijazo ili kuwezesha mashauriano katika juhudi za kufanyia marekebisho tume hiyo. Akiongea kwenye kanisa la jeshi la wokovu kwenye eneo bunge la Turbo kaunti ya Uasin Gishu ambako alihudhuria ibada ya Jumapili, Ruto aliwaambia viongozi wakubali mashauriano ili kuunganisha jamii mbalimbali nchini. Aliwahimiza viongozi kukomesha siasa duni na kuungana katika ujenzi wa taifa.