Naibu Rais atoa wito wa uwazi na uwajibikaji katika sekta ya uchimbaji madini

Naibu wa Rais William Ruto ametoa wito wa uwazi na uwajibikaji katika sekta ya uchimbaji madini ili kuepusha taarifa potovu ambazo huenda zikasababisha mizozo katika jamii zinazoishi kwenye maeneo yenye madini. Naibu wa Rais alisema utajiri wa madini nchini ni mali ya wakenya na unapaswa kutumiwa kuwatajirisha wananchi. Ruto alisema sheria ya madini inamaliza mizozo kuhusu ugavi mapato ya madini ikieleza kwamba asilimia 10 ya mapato hayo yataendea jamii ambako madini hupatikana.

Akiongea wakati wa mkutano kuhusu uchimbaji madini nchini uliowaleta pamoja wadau katika sekta ya uchimbaji madini, Ruto alisema serikali imeanzisha mpango wa ugavi mrabaha wa mapato ya madini kwa kiwango cha 70:20:10 kati ya serikali ya kitaifa, serikali ya kaunti na jamii. Naibu wa Rais alisema ipo haja ya kufanya mazungumzo zaidi kuhusu ongezeko la ukuaji, mabadiliko na uwekezaji katika sekta ya uchimbaji madini. Alisema rasilmali za madini za nchi zinapaswa kutumika kwa njia nzuri ili faida yake inufaishe vizazi vijavyo.