Naibu Rais asema serikali imejitolea kulinda haki ya kikatiba ya kila mmoja

Naibu Rais, William Ruto, amewahakikishia wakenya kwamba serikaliA� imejitolea kulinda haki ya kikatiba ya kila mmoja wao kushiriki katika uchaguzi wa viongozi. Akigusia miito ya upinzani ya kususia uchaguzi ikiwa tume ya IEBC haitatekeleza marekebisho wanayotaka, Ruto alisema hakuna yeyote aliye na mamlaka ya kuwanyima wakenya haki yao ya kupiga kura. Alihimiza upinzani kuacha kuchafulia sifa tume ya IEBC, na badala yake kuelekeza juhudi zao kwa kampeini. Akiongea wakati wa kumpokea aliyekuwa makamu mwenyekiti wa chama cha ODM, Paul Otuoma, -katika chama cha Jubilee Ruto alimtaka kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, kuheshimu utawala wa sheria. Wakati huo huo; Ruto alionya wale wote walio na nia ya kuharibu mali ya kibinafsi kwamba watakabiliwa vilivyo kisheria. Viongozi walioandamana na naibu Rais waliahidi kuhakikisha anapata kura nyingi zaidi kutoka eneo hilo la Magharibi mwa Kenya.