Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa Kuhusu Maswala ya Jinsia ya Usawa, Winfred Lichuma…

MWENDE-CUTS

 

Mwenyekiti wa tume ya kitaifa kuhusu maswala ya jinsia na usawa, Winfred Lichuma amemhimiza mwanasheria mkuu profesa Githu Muigai kuanzisha utaratibu wa kutekeleza kifungu cha 34 cha sheria kuhusu dhuluma za kijinsia ya mwaka 2015.

Sheria hiyo inaratibu kinga, fidia na malipo kwa waathiriwa wa dhuluma za kijinsia. Lichuma alisema kanuni na utaratibu wa utekelezaji sheria hiyo hazijaidhinishwa, hatua ambayo inawanyima haki waathiriwa wa dhuluma za kijinsia.

Aidha tume hiyo inapendekeza marekebisho kwenye sheria hiyo ili kutoa fulsa ya kubuni vituo vya kutoa hifadhi kwa wahanga na manusura wa dhuluma za kijinsia. Lichuma alimtaka Inspekta Jenerali wa Polisi kuhakikisha uchunguzi wa kina wa visa vya dhuluma za kijinsia unafanywa haraka iwezekanavyo ili wahanga wa visa hivyo wapate haki.

Wakati huo huo, Jackline Mwende atapokea mikonoA� bandia kutoka kwa hospitali ya Kikuyu ya kanisa la PCEA. Mwende alikatwa mikono na mumewe aliyemshutumu kwa kutomzalia watoto. Operesheni ya kumpachika mikono bandia imedhaminiwa na shirika la kutetea haki za wanawake la Merck kutoka Ujerumani na mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Taita Taveta, Joyce Lay aliyewaongoza viongozi wengine wa kike kumtembelea Mwende nyumbani

Mwende ambaye hakuendelea na masomo baada ya kufanya mtihani wa darasa la nane pia atapata ufadhili wa kumwezesha kuendelea na masomo kutoka chuo kikuu cha Methodist ilhali serikali ya kaunti ya Machakos na shirika la Merck yampa marupurupu ya shilingi elfu-30 na elfu-25 mtawalia kila mwezi.
Viongozi wa kina mama wakishirikiana na chama cha wanasheria wa kike hapa nchini wametoa wito wa kuchukua hatua kali za sheria dhidi ya mumewe Mwende, Stephen Ngila.
Mwenyekiti wa chama hicho Josephine Mung’are amesema chama hicho kimepata wakili atakayetoa usaidizi wa sheria kwa Mwende.