Mwanzo Mpya Wa FKF

Mwenyekiti wa timu ya Kariobangi Sharks, mwenye umri wa miaka 37, Nick Mwendwa, jana alichaguliwa mwenyekiti mpya wa shirikisho la soka humu nchini. Mwendwa alijipatia kura 50 kati ya 77, huku mwenyekiti wa Gor Mahia Ambrose Rachier, akiridhika na nafasi ya pili kwa kura 27 kwenye uchaguzi wa taifa ulioandaliwa katika ukumbi wa Kasarani wa michezo ya ndani.

Mgombea mwenza Doris Petra amechaguliwa naibu mwenyekiti baada ya kujipatia jumla ya kura 54 kati ya 55 baada ya kupambana katika raundi ya pili na Dan Shikanda aliyepata kura moja na Andrew Amukowa ambaye hakupata kura. Katika raundi ya kwanza, Petra alikuwa amepata kura 36, Dan Shikanda kura 13 na Andrew Amukowa kura 21.

Uchaguzi huo uliofanywa kwa njia ya amani na ambao wawaniaji wote walikubali matokeo hayo unaipatia taifa hili fursa ya kukuza talanta na kuinua viwango vya soka humu nchini.

Changamoto kuu kwa Nick Mwendwa na wenzake ni kuibadilisha ligi kuu ya soka humu nchini kuwa na timu 18 kutoka timu 16, tatizo lililomkumba aliyekuwa mwenyekiti Sam Nyamweya alipokua uongozini.