Mwaniaji wa upinzani Maldives adai kuwa mshindi katika uchaguzi

Mwaniaji wa muungano wa upinzani nchini Maldives amedai kuibuka mshindi katika uchaguzi ulioandaliwa nchini humo.  Ibrahim Mohamed Solih amedai ana uongozi ambao hauwezi kufikiwa na Abdulla Yameen huku kura zikiwa zimehesabiwa katika masanduku 437 kati ya masanduku 472 kwa mujibu wa vyombo vya habari katika kisiwa hicho kilichoko katika eneo la bahari Hindi.

Hata hivyo tume ya kitaifa ya uchaguzi nchini humo haijatangaza matokeo rasmi. Wachunguzi walisemekana kuamini kuwa kulikuwa na udanganyifu katika uchaguzi huo ili kumpendelea Yameen ambaye anasemekana kuwa na uhusiano wa karibu na Uchina huku Solih akisemekana kuegemea India.  Serikali ya rais Yameen inalaumiwa kwa kuwanyamazisha na kuwahangaisha wapinzani.

Polisi walivamia makao makuu ya upinzani mkesha wa siku ya uchaguzi.  Jumuiya ya ulaya na Marekani zimeelezea wasiwasi kuhusu uchaguzi huo huku zikitishia kuweka vikwazo iwapo hali ya demokrasia haitaimarika nchini humo.