Mwanaume Ahukumiwa Kifungo Cha Maisha Gerezani Kwa Kuuza Pembe Za Ndovu

Mahakama ya Nyahururu imemhukumu mwanamume mmoja kifungo cha maisha gerezani baada ya kukiri kosa la kuuza pembe za ndovu. James Ewoi aliye na umri wa miaka 31 alikiri makosa ya kupatikana na vipande vitatu vya pembe za ndovu na kuendesha biashara hiyo. Hakimu mkuu Peter Ndege, alimpa Ewoi muda afikirie uamuzi wake kabla ya kusomewa tena mashtaka yaliyomkabili. Aliagizwa alipe faini ya shilingi milioni-3 kwa kupatikana na bidhaa hizo za serikali, na nyingine ya shilingi milioni-20 kwa kujihusisha na biashara hiyo haramu. Mshukiwa huyo alikamatwa katika eneo la ADC Mutara alipokuwa akiuza kilo-6 za vipande vya pembe za ndovu vinavyokisiwa kugharimu shilingi milioni 1.3. Hata hivyo, mahakama ilifahamishwa kwamba mnamo tarehe 13 mwezi Machi mwaka huu, mwananchi mmoja aliwafahamisha maafisa wa polisi kwamba Ewoi alikuwa akitafuta mnunuzi wa pembe hizo. Kisha maafisa wa shirika la huduma kwa wanyama pori walimfumania mshukiwa kwa kujisingizia kuwa wangenunua bidhaa hizo kwa shilingi million 1.3. Kwa mujibu wa sheria, mtu yeyote anayepatikana na kosa la uwindaji haramu na kuendesha biashara ya bidhaa za wanyama pori anafaa kuhukumiwa kifungo cha maisha gerezani au faini isiyopungua shilingi milioni-20 au vyote viwili. Ewoi hangemudu faini hiyo kwa hivyo alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani. Hakimu huyo alisema mshukiwa ana siku-14 kukata rufaa.