Mwanamuziki maarufu Joseph Kamaru aaga dunia

Mwanamuziki maarufu wa mtindo wa densi wa Benga Joseph Kamaru amefariki dunia. Kamaru, mwenye umri wa miaka 79 aliaga dunia alipokuwa akitibiwa katika hospitali ya MP Shah hapa Nairobi. Kwa mujibu wa mwanawe wa kiume Stephen Maina, mwanamuziki huyo alikata roho jana usiku kutokana na matatizo ya kupumua. Kamaru, ambaye alizaliwa huko Kangema, kaunti ya Murang’a alianza uimbaji mnamo mwaka wa 1956. Wakati wa kipindi cha usanii kilichodumu miaka 44, Kamaru mbali na kutunga nyimbo kadhaa ziliovuma hasa sana katika lugha ya Kikuyu, alitokea kuwa maarufu sana katika ulimwengu wa muziki hapa nchini na hata ng’ambo. Alikuwa kitovu cha tunu ya utamaduni wa waKikuyu.

Miongoni mwa nyimbo maaarufu alizotunga ni Ndari ya Mwalimu,Tiga kuhenia na Nuu ucio. Muziki wake ulipendwa na watu wa tabaka zote, wakiwemo wasomi. Kwa wakati mmoja alikuwa na uhusiano wa karibu na hayati rais Jomo Kenyatta na vile vile rais mstaafu Daniel Arap Moi, kabla ya kutofautiana na uongozi kutokana na sababu za kisera.