Mwanamke asombwa na mafuriko Syokimau

Mwanamke wa umri wa makamo alifariki aliposombwa na mafuriko katika eneo la Syokimau kwenye barabara kuu ya Mombasa. Yasemekana mwanamake huyo alikuwa akijaribu kupitia kwenye mafuriko alipoteleza kwenye mtaro na kusombwa.

Mwili wa marehemu ulipatikana leo asubuhi. Mvua kubwa iliyonyesha katika kaunti za Nairobi na Machakos jana jioni pia ilisababisha mafuriko na msongamano mkubwa wa magari katika barabara ya Mombasa. Katika sehemu ya Syokimau mstawishaji ambaye alikuwa amejenga ukuta katika sehemu ambako maji yanapitia akisubiri kujenga nyumba ya orofa anakadiria hasara baada ya ukuta huo kubomolewa na mafuriko na mali ya thamani isiojulikana kuharibiwa.

Wakazi wa sehemu hiyo iliyoko katika kaunti ya Machakos sasa wanatoa wito kwa maafisa husika kubomoa majengo yaliyokitwa katika mapito ya maji wakisema yanasababisha mafuriko katika eneo hilo. Barabara nyingi katika sehemu hiyo sasa hazipitiki kufuatia mvua kubwa inayonyesha.

Kwingineko, wafanyabiashara katika eneo la kati kati ya mji wa Kisii walipata hasara kubwa baada ya bidhaa zao kusombwa na mafuriko ya ghafla yaliokumba soko kubwa zaidi la wazi katika eneo hilo. Mafuriko hayo yalitokana na kufurika kwa mto Nyakomiraso.

Afisa mkuu wa wa kukabiliana na mikasa katika kaunti ya Kisii, Patrick Lumumba alisema hakukuwa na majeruhi. Hata hivyo aliwalaumu wafanyabiashara kwa kupuuza onyo lililotolewa awali kuhusu mvua ya El-Nino.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *