Mwanamke Afa Katika Kambi Ya Polisi South B Huku Kukiwa Na Madai Ya Ubakaji

Polisi wanachunguza tukio ambapo mwanamke mmoja alifariki dunia alipokuwa akizuiliwa kwenye kambi ya polisi wa utawala ya Mariguini katika mtaa wa South B, jijini Nairobi huku kukiwa na madai kwamba huenda alibakwa.

Mwishoni mwa juma, wakazi wa mtaa wa South B waliandamana na kufunga barabara baada ya kufahamishwa kuhusu kifo cha mwanamke huyo Mercy Nanjala wakidai alinyimwa ruhusa ya kutafuta huduma za matibabu licha ya hali yake kuzorota.

Ilidaiwa kwamba alifariki alipokuwa akipokea matibabu kutokana na matatizo ya kiafya yaliyomkumba wakati alipozuiliwa kwenye kituo hicho cha polisi kwa saa tisa.

Nanjala alizuiliwa baada ya rafiki yake, Emily Wasike, ambaye kwa sasa ametoweka kudai kwamba aliiba simu yake ya rununu.

Afisa mkuu wa polisi wa utawala katika eneo la Makadara John Macharia amekiri kwamba Nanjala alikuwa amezuiliwa katika kituo hicho. Uchunguzi umeanzishwa ili kubainisha ni kwa nini hakuhamishwa hadi rumande ya kituo cha polisi cha Industrial Area. Kulingana na afisa mkuu wa polisi katika kaunti ya Nairobi Japheth Koome uchunguzi pia umeanzishwa kubainisha madai kwamba Nanjala alibakwa na kudhulumiwa alipokuwa akizuiliwa kwenye kambi hiyo.