Mwalimu mkuu akamatwa kwa kuchelewa na kuwa mlevi

Mwalimu mkuu wa shule moja ya sekondari huko Gilgil, katika kaunti ya Nakuru amekamatwa baada ya kuwasili kuchelewa na akiwa mlevi katika kituo kimoja cha usambazaji wa karatasi za mtihani wa KCSE katika kaunti hiyo.Christopher Maisiba,ambaye ni mwalimu mkuu wa shule ya secondari ya Mawaka ambaye alikuwa ameenda katika kituo hicho kuchukua karatasi za mtihani wa masomo ya Isibati na biolojia alipigwa na butwaa alipokutana na afisa mkuu mtendaji wa tume ya kuwaajiri walimu nchini Nancy Macharia akisimamia shughuli ya ugavi wa karatasi za mtihani katika kituo hicho. Macharia alishangazwa na hali ya mwalimu huyo mkuu aliyeonekana kuyumba yumba alipoenda kuchukua karatasi za shule yake za mtihani huo. Maisiba,hata hivyo alisisitiza kwamba hakuwa mlevi huku akisema alilazimika kwenda katika kituo hicho haraka kuchukua karatasi hizo kabla ya kuelekea katika kituo chake cha kazi. Kamishna wa kaunti ya Nakuru, Joshua Nkanatha, aliwaagiza polisi kumkamata mwalimu huyo. Macharia alimuagiza afisa wa ubora wa elimu katika kaunti ndogo ya Gilgil kuchukua karatasi hizo ya mtihani na kuzipeleka katika shule hiyo.