Muungano wa Jubilee na KANU wasitishwa

Mkataba wa kubuni muungano kati ya chama cha Jubilee na kile cha KANU umesimamishwa.

Kulingana na jopo la kutatua mizozo ya vyama vya kisiasa, agizo hilo litadumu hadi kamati Kuu ya kitaifa ya chama cha Jubilee itakapoidhinisha mkataba huo.

Jopo hilo limesema kuwa mkataba huo unafaa kuidhinishwa na kamati Kuu ya kitaifa ya chama cha Jubilee chini ya kanuni za Usajili wa Vyama vya kisiasa.

Jopo hilo limesema kuwa mkataba huo ulikiuka sheria kuhusu usajili wa vyama vya kisiasa, na kifungu cha 21 cha sheria kuhusu Usajili wa Vyama vya Kisiasa ya mwaka 2019.

Wabunge watatu wa chama cha Jubilee, Caleb Kositany wa eneo bunge la Soy, seneta wa Nakuru, Susan Kihika, mbunge wa Mumias Mashariki, Benjamin Washiali na Mweka Hazina wa chama cha Jubilee, Albert Mutai, waliwasilisha malalamishi kwa jopo hilo wakitaka kujua uhalali wa mkataba huo.

Vyama vya Jubilee na KANU vimetajwa kama pande husika kwenye kesi hiyo.

Kwenye mkutano wa chama hicho uliowaleta pamoja maseneta kutoka chama chama hicho na kile cha KANU jumatatu, seneta wa kaunti ya Pokot Magharibi, Samuel Poghisio alichaguliwa kuwa kiongozi wa walio wengi katika bunge la seneti na kuchukua nafasi ya Kipchumba Murkomen wa Elgeyo Marakwet.