Muungano Wa CORD Wasimamisha Kwa Muda Maandamano Dhidi Ya IEBC

Muungano wa CORD umesimamisha kwa muda maadamano yake ya kila wiki dhidi ya tume huru ya uchaguzi na mipaka-IEBC. Upinzani umeipatia serikali siku-10 kujibu miito yake ya kufanywa kwa majadiliano. Kwenye taarifa ya pamoja iliyowasilishwa jana maseneta James Orengo na Johnstone Muthama walisema uamuzi wa kusimamishwa kwa maandamano hayo utatoa nafasi ya majadiliano katika juhudi za kusuluhisha mzozo kuhusu makameshina wa Tume ya IEBC kwa njia ya maelewano. Viongozi wa muungano wa CORD hata hivyo wameonya kwamba watarejelea maandamano hayo katika muda wa majuma mawili endapo serikali ya Jubilee haitaandaa majadiliano na upinzani ili kuamua mwelekea kuhusu swala hilo.
Kwingineko katika majengo ya Bunge,baadhi ya wabunge kutoka eneo la Nyanza wameagiza kuhamishwa mara moja kwa maafisa wote wakuu wa polisi katika kaunti za Kisumu,Siaya,Homabay na Migori. Wabunge hao wameagiza hayo kufuatia dhuluma zinazodaiwa kutekelezwa na polisi dhidi ya waandamanaji ambapo watu watatu waliuawa. Wakiongozwa na mbunge wa Suba John Mbadi,wabunge hao waliwashutumu maafisa wa polisi kwa kuwafyatulia risasi waandamanaji ili kuwatawanya.