Muungano Wa CORD Waapa Kuwatimua Makamishna Wa IEBC

Seneta wa Mombasa Hassan Omar amesema kwamba muungano wa Cord umejitolea kuhakikisha kwamba makamishna wa tume ya IEBC wanafutwa kazi kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao. Alisema kuwa tume hiyo haiwezi kutegemewa kuandaa uchaguzi wa haki. Alidai kwamba tume hiyo inakabiliwa na kibarua kigumu cha kulinda uadilifu wake na inachochea mzozo na ukosefu wa uthabiti. Akiongea mjini Mombasa wakati wa sherehe ya kwanza ya kimataifa ya kitamaduni ya jamii ya Wanubi iliyohudhuriwa na naibu waziri mkuu wa Uganda Moses Ali, Omar alisema kuwa tume ya IEBC inayoongozwa naA� Issak Hassan haiwezi kuaminika kusimamia uchaguzi mkuu ujao. Alidai kuwa tume hiyo imejiruhusu kushawishiwa na muungano tawala. Hivyo basi alisema haiwezi kutegemewa kuandaa uchaguzi ambao unaakilisha matakwa ya wapigaji kura wengi nchini.