Mututho Ataka Viongozi Wa Wanafunzi Wa Chuo Kikuu Cha Nairobi Wachunguzwe Kuhusiana Na Mihadarati

Mwenyekiti wa shirika la NACADA John Mututho sasa anataka viongozi wa wanafunzi katika chuo kikuu cha Nairobi wachunguzwe kuhusiana na matumizi na uuzaji wa mihadarati katika chuo hicho. Mututho alikariri kwamba uuzaji wa dawa za kulevya umezidi katika chuo hicho ambacho kilifungwa wiki iliyopita kufuatia siku mbili za gasia za wanafunzi. Wito huo umetolewaA� wiki moja baada ya Inspekta Jenerali wa polisi Joseph Boinett kuagiza kwamba Mututho aandikishe taarifa kwa polisi kuhusiana na madai yake. Licha ya agizo hilo, Mututho alisema kwamba maafisa muhimu wa serikali wana taarifa zote na akashangaa ni kwanini hakuna hatua iliyochukuliwa. Akiwahutubia wanahabari huko Naivasha, Mututho alilitaja janga la mihadarati katika chuo hicho kuwa lakutia wasi wasi akiongeza kwamba hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa. Alimpongeza Naibu wa chansela wa chuo hicho kwa kukiri kuwa matumizi ya mihadarati yapo akisema kwamba wakati umewadia wa hatua muhimu kuchukuliwa.