Mutula Kilonzo akashifu kanda ya video inayodaiwa kukejeli jamii ya wakamba

Seneta wa makueni Mutula Kilonzo Junior ameandikia barua tume ya uwiano na utangamano wa taifa na ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma kuchukua hatua za kisheria dhidi ya kanda ya video ya muzikiA� ya Isaiah inayojulikana kama Ikamba iliyotayarishwa na Davinex Pictures na inayomuangazia Waharaka. Wimbo huo ambao umeimbwa kwa lugha ya kikuyu unadaiwa kutumia lugha ya kejeli la kudhalalisha dhidi ya jamii ya Wakamba huku ukimlenga gavana wa Kitui, Charity Ngilu katika juhudi zake za kupiga marufuku uchomaji makaa katika kaunti hiyo. Mutula Junior anasema wimbo huo unalenga kuzua uhasama kati ya jamii za Wakamba na Wakikuyu. Kulingana na seneta huyo, wimbo huo unadai kwamba Wakamba kwa sasa wanafurahia kula maembe na hivi karibuni watakuwa wakila mbwa baada ya msimu wa maembe kukamilika. Mwenyekiti wa tume ya utangamano na uwiano wa kitaifa Francis ole Kaparo alisema wanachunguza wimbo huo. Afisa mkuu wa bodi ya kuorodhesha filamu nchini , Ezekiel Mutua pia alishtumu wimbo huo akisema wanamuziki hao wawili sharti washtakiwe.