Muthama aenda mahakamani kupinga uamuzi wa serikali kusimamisha matumizi ya pasipoti

Seneta wa zamani wa Machakos Johnstone Muthama amekwenda mahakamani kupinga uamuzi wa serikali wa kusimamisha matumizi ya hati za usafiri za pasipoti za viongozi wa muungano wa NASA. Seneta huyo wa zamani anaitaka mahakama kumzuia mkurugenzi wa Idara ya uhamiaji Gordon Kihalangwa kufutilia mbali stakabadhi yake ya utambulisho. Muthama ni miongoni mwa viongozi 14 wa upinzani waliopewa muda wa siku 14 na idara ya uhamiaji kusalimisha hati zao za pasipoti na wakikosa hati hizo zifutiliwe mbali. Wakati huo huo mahakama hiyo iliongeza muda hadi Machi 20 wa maagizo ya kuwazuia polisi kuwakamata ama kuwahangaisha wanahabari watatu wa kampuni ya Nation Media. Justice Luka Kimaru akiongeza muda wa dhamana yao alisema kwamba wanahabari Linus Kaikai, Larry Madowo na Ken Mijungu wanahitaji kulindwa kwa kuishi kwa hofu ya kukamatwa. Upande wa mashtaka ulipinga kuongezwa kwa muda huo wa dhamana kwa wanahabari hao watatu na badala yake wakawasilisha ombi la kutaka agizo hilo liondolewe ukidai kwamba polisi hawana mpango wa kuwakamata wanahabari ili kuhojiwa.