Musalia Mudavadi Asifia Kujitolea Kwa Baadhi Ya Makamishna Wa IEBC Kujiuzulu

Kiongozi wa chama cha Amani National Congress Musalia Mudavadi amesifia kujitolea kwa baadhi ya makamishna wa tume huru ya uchaguzi na mipaka-IEBC kujiuzulu. Mudavadi anamhimiza rais Uhuru Kenyatta kuridhia matakwa ya makamishna hao ili kufanikisha kutatuliwa kwa mzozo unaokumba tume hiyo. Kwenye taarifa, Mudavadi alipongeza makamishna hao watano kwa kudhihirisha uzalendo na akawahamiza wale watano waliosalia kujiuzulu pia. Mudavadi alieleza matumaini kuwa kamati teule ya wanachama 14 waliopendekezwa watatatua mzozo huo na kuleta marekebisho yafaayo kwenye mfumo wa uchaguzi hapa nchini. Duru zinadokeza kuwa makamishna Yusuf Nzibo, Albert Bwire, Kule Galma Godana na Abdullahi Sharawe walimwandikia arifa rais Uhuru Kenyatta Jumanne iliyopita wakieleza kujitolea kwao kujiuzulu. Makamishna wengine watano akiwemo mwenyekiti wa tume hiyo Issack Hassan wameapa kuwa hawatabanduka.