Musalia Mudavadi aitaka serikali kutatua mzozo kuhusu mishahara ya wahadhiri

Kinara mwenza wa muungano wa Nasa Musalia Mudavadi, ameitaka serikali kutatua mzozo kuhusu mishahara ya wahadhiri wa vyuo vikuu. Musalia aliongeza kuwa mvutano baina ya wahadhiri hao na serikali utatatiza wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na vyuo vikuu mwezi Mei, kutokana na mgomo wa wahadhri hao ambao sasa umeingia katika mwezi wake wa pili. Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari,kinara huyo wa chama cha ANC aliishauri serikali kuvifunga vyuo hivyo vikuu vya umma hadi mzozo huo utakapotatuliwa.Mzozo huo wa sasa umechochewa na kushindwa kwa wizara za elimu na fedha ,tume ya mishahara na marupurupu pamoja na jopo la pamoja la ushauri la vyuo vikuu kuwasilisha pendekezo mbadala kuhusu mishahara hiyo kama ilivyoagizwa na mahakama, ili kutoa fursa ya majadiliano kuhusu mishahara hiyo.Chama cha wahadhiri pamoja na kile cha wafanyikazi wa vyuo vikuu vimeapa kudumisha mgomo huo hadi matakwa yao yatakapo shughuilikiwa.