Murkomen na Kihika Wang’olewa

Bunge la Seneti limetekeleza mabadiliko katika uongozi wa chama cha Jubilee ambayo yamesababisha Seneta wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet  Kipchumba Murkomen kuondolewa kwenye wadhifa wa kiongozi wa wengi na wadhifa huo kupatiwa seneta wa Pokot Magharibi Samuel Poghisio wa chama cha KANU.

Seneta wa  Nakuru  Susan Kihika pia ameondolewa kwenye wadhifa wa kiranja wa walio wengi na nafasi yake kupatiwa seneta wa Muranga Irungu Kangata.

Mabadiliko hayo yametekelezwa licha ya jopo la utatuzi wa mizozo ya vyama vya kisiasa kusimamisha kwa muda muungano kati ya chama cha Jubilee na kile cha KANU.

Spika wa bunge la seneti Ken Lusaka aliidhinisha mabadiliko hayo jinsi yalivyopokelewa na kuahidi kutoa uamuzi wa kina baadaye. Hata hivyo alisema aliridhika kuwa utaratibu mwafaka ulizingatiwa katika kufanya mabadiliko hayo.  

Lusaka alisema ujumbe huo uliwasilishwa na stakabadhi zote zinazohitajika miongoni mwao nakili za mkutano wa wabunge wa chama cha Jubilee.

Lusaka alisema kuwa alipokea pia orodha ya maseneta iliyotiwa saini ambao walihudhuria mkutano huo katika ikulu ya Nairobi .  

Murkomen alipinga mabadiliko hayo akisema yalifanywa kwa nia mbaya na kumtuhumu spika kwa kukubali kushurutishwa kuidhinisha mabadiliko hayo.  

Matamshi hayo hata hivyo yalimkera kiongozi wa walio wachache katika bunge la seneti James Orengo ambaye alimkosoa Murkomen kwa kuhujumu mamlaka ya spika na kukosa kumheshimu rais.