Mudavadi,Wetangula wataka IEBC iundwe upya

Kiongozi wa chama cha Amani Musalia Mudavadi, na mwenzake wa Ford Kenya, Moses Wetang’ula sasa wanataka tume huru ya uchaguzi na mipaka-IEBC iundwe upya kabla ya kuandaliwa kwa kura ya maamuzi.

Akiongea na wanahabari katika kaunti ya Bungoma, viongozi hao wawili walidai kwamba wakenya hawana imani na tume ya IEBC jinsi ilivyo kwa sasa. Walidai kwamba kuna mkanganyiko na kukata tamaa katika tume ya IEBC, ambapo walitaka iundwe upya kabla ya kusimamia kura ya maamuzi.

Kwa upande wake Wetang’ula aliwakosoa wale wanaoshinikiza kuharakishwa kwa kura ya maamuzi, akikariri kwamba wakenya sharti wapewe muda wa kuchunguza marekebisho yanayopendekezwa.  Alidai kwamba baadhi ya viongozi hawaaminiki katika shinikizo zao za kutaka katiba irekebishwe, akisema wanapania kujitengea nyadhifa za uongozi.