Mudavadi Atarajiwa Kuhudhuria Kongamano La Chama Cha Democratic Mjini Philadephia

Kiongozi wa chama cha Amani National Congress, Musalia Mudavadi ataelekea nchini Marekani leo usiku kuhudhuria kongamano la chama cha Democratic mnamo tarehe-25 mwezi huu mjini Philadephia. Kongamano hilo linatarajiwa kumuidhinisha rasmi Hillary Clinton kuwa mgombeaji urais wa chama hicho. Mudavadi ataungana na viongozi wengine kutoka kote duniani ambao watahudhuria kongamano hilo. Hapo jana, wanachama wa chama cha Republican walimuidhinisha rasmi Donald Trump kuwa mgombeaji urais wa chama hicho wakati wa kongamano lao lililoandaliwa mjini Cleveland, Ohio. Mudavadi pia atakuwa mgeni kwenye kikao cha viongozi mbali mbali ambacho kitaandaliwa na taasisi ya kitaifa kuhusu Demokrasia kitakachojumuisha wabumnge wote wa chama cha Democratic. Adiha, Mudavadi atakuwa kwenye jopo la kujadili mbinu za kuendesha kampeni ya urais ambalo litajumuisha aliyekuwa waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Marekani, Madeleine Albright ambaye ni mwenyekiti wa taasisi ya Demokrasia nchini Marekani na spika wa zamani, Tom Daschle. Mudavadi huenda akakutana na rais Barack Obama kwenye kongamano hilo ingawa ratiba yake inaashiria kuwa ataelekea mjini Washington baada ya kuhudhuria kongamano la Philadelphia kwa mashauriano na viongozi mbali mbali.