Mtu Mmoja Afariki Baada Ya Mapigano Kuzuka Transmara

Mtu mmoja alifariki alipofumwa na mshale kufuatia mapigano ya kijamii yaliozuka upya katika eneo la Transmara kwenye mpaka kati ya kaunti za Kisii, Narok na Kericho. Watu sita zaidi wamelazwa hospitalini huko Keroka na Litein baada ya kufumwa mishale wakati wa ghasia hizo zilizochochewa na jaribio la wizi wa mifugo lililotibuka. Mwanamke mmoja pia amelazwa katika hospitali ya Litein baada ya kupigwa risasi kimakosa na maafisa wa usalama waliokuwa wakikabiliana na vijana waliojihami. Nyumba kadhaa ziliteketezwa na migomba ya ndizi kuharibiwa katika maeneo ya Ikorongo na Olmemil. Maafisa zaidi wa usalama wamepelekwa katika eneo hilo kurejesha utulivu. Ghasia hizo zimehusishwa na mzozo wa ardhi. Maafisa wa serikali ya kitaifa kutoka kaunti za Narok na Kisii walitembelea eneo hilo na wanatarajia kuandaa mikutano ya amani baina ya jamii zinazozozana. Kamishna wa kaunti ya Kisii, Kula Hache aliliambia shirika la utangazaji la Kenya- KBC kwa njia ya simu kuwa mkutano wa hadhara utaandaliwa kwenye eneo hilo hapo kesho. Wakazi wanadai kuwa ghasia hizo zinatokana na visa vya wizi wa mifugo, mzozo wa ardhi na uhalifu wa kawaida miongoni wa vijana.