Mtaala mpya wa elimu kuanza Januari mwakani

Mtalaa mpya wa elimu wa 3-6-6-3 utaanza mwezi Januari mwaka ujao na huku ule wa 8-4-4 ulioanzishwa mwaka 1985 ukifikia kikomo. Hata hivyo ikiwa imesalia miezi michache kabla ya wakati huo chama cha wachapishaji vitabu nchini kimetoa wito kwa serikali kutoa pesa za kutosha kwa wizara ya elimu ili kuziwezesha shule kununua vitabu vya kutosha kufanikisha mfumo huo mpya. Akiwahutubia wanahabari kabla ya makala ya 20 ya maonyesho ya kimataifa ya vitabu jijini Nairobi mwenyekiti wa chama hicho Lawrence Njagi alisema kuwa mtalaa huo mpya ambao unahimiza ushindani unahitaji kila mwanafunzi kuwa na vitabu vyake. Njagi amesema kuwa ufanisi wa nchi hii katika elimu unahusiana moja kwa moja na ubora wa elimu kuanzia kiwango cha kimsingi hadi kile cha juu zaidi.