Mswada Mpya Watekelezwa Na Tume huru Ya IEBC Kuimarisha Usajilishaji Wa Wapiga Kura

Katika juhudi za kuongeza idadi ya wapiga kura watakaoshiriki kwenye uchaguzi mkuu ujao, tume huru ya uchaguzi na mipaka imesema itaimarisha shughuli ya kuwasajili wapiga kura kati ya tarehe 15 mwezi huu na tarehe 15 mwezi Machi mwaka huu.Kwenye taarifa, mwenyekiti wa tume hiyo Issack Hassan amesema tume hiyo pia itaandaa shughuli sawa na hiyo mwakani hata ingawa uandikishaji wa wapiga kura utaendelea kwenye maeneo bunge hadi mwezi Mei mwaka ujao wakati sajili ya wapiga kura itakapofungwa.Hassan alisema tume hiyo imewaajiri wahudumu 5,756 watakaoendeleza shughuli hiyo inayofadhiliwa na wizara ya fedha kwa ushirikiano na wafadhili wa kimaendeleo.Aidha tume hiyo imewaaajiri maafisa 290 wenye ujuzi wa teknolojia ya mawasiliano watakaohudumu kwenye makao makuu na pia katika maeneo ya nyanjani.Vifaa 5,756 vya kuwasajili wapiga kura kielektroniki vitapelekwa kwenye wodi 1,450 huku kukiwa na vituo 24,559 vya usajili.