Msichana mwenye Umri wa Miaka 5 Afariki kwenye moto Huko Kitengela

Msichana mwenye umri wa miaka mitano amechomeka hadi akafariki kwenye moto uliozuka katika makazi yao huko Kitengela. Duru zadokeza kwamba mtoto huyo alikuwa ameachwa chini ya utunzi wa dadake mkubwa mwenye umri wa miaka 8 na alikuwa amelala wakati moto huo ulipozuka.

Kulingana na majirani moto ulionekana ndani ya nyumba za wahudumu wasio wahadhiri wa chuo kikuu cha East Africa. Juhudi za majirani za kumuokoa msichana huyo hazikufua dafu kwani moto huo ulienea haraka ndani ya nyumba hiyo iliyojengwa kwa mabati.

Mwili wa mwanafunzi huyo wa darasa la kwanza ulichomeka hivi kwamba haungetambulika. Akithibitisha kisa hicho afisa mkuu wa polisi huko Isinya, Steve Weda, alitaja kisa hicho kuwa cha kusikitisha. Aliwahimiza wazazi kuwa waangalifu na wawe wakiwaacha watoto wao chini ya utunzi wa watu wazima.