Mshindi Wa Uchaguzi Nchini Gambia Ana Matumaini Ya kuapishwa

Mshindi kwenye uchaguzi wa urais nchini Gambia, Adama Barrow amesema anatumaini kuwa ataapishwa wiki ijayo licha ya raisA´┐ŻYahya Jammeh kukataa kubanduka uongozini. Hatamu ya rais Jammeh itakamilika rasmi jumatano wiki ijayo. Rais huyo amewasilisha rufaa mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi huo. Viongozi kutoka nchi za shirika la ECOWAS wanatarajiwa kuelekea nchini Gambia kujaribu kumshawishi rais Jammeh kukabidhi mamlaka kwa mshindi wa uchaguzi huo. Shirika la ECOWAS limeonya kuwa huenda likatumia nguvu za kijeshi kumuondoa mamlakani rais Jammeh ikiwa atakatalia uongozini. Aidha, Barrow amemhimiza rais Jammeh kuheshimu katiba ya nchi hiyo akisema mashauriano baina yao yatasaidia kukomesha uhasama katika taifa hilo la Afrika Magharibi. Wakili wa Jammeh jana aliwasilisha rufaa mahakamani kupinga kuapishwa kwa Barrow. Jammeh aliyeingia mamlakani kupitia mapinduzi ya kijeshi ameitawala nchi hiyo kwa miaka-22 na alikuwa amekubali matokeo hayo ya uchaguzi kabla ya kubadili uamuzi huo.