Mshauri Wa Rais Wa Gambia Adai Zaidi Ya Milioni 11 Zimetoweka

Mshauri wa rais wa Gambia  Adama Barrow amesema kuwa zaidi ya dola milioni 11 zimetoweka kutoka hazina ya kitaifa na inaaaminika zimeporwa na aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo  Yahya Jammeh.Mai Ahmad Fatty  amesema kuwa wataalamu wa  maswala ya kifedha wangali wanajaribu kukadiria kiasi kamili cha pesa zilizoibwa kutoka hazina ya taifa hilo.Miongoni mwa tunu ambazo inadaiwa Jammeh amepora kutoka Gambia ni pamoja na magari ya anasa na pesa.Imearifiwa kuwa mali hiyo ilipakiwa kwenye ndege ya kubeba mizigo ya Chad usiku ambao Jammeh aliondoka kutoka nchi hiyo.Kwa mujibu wa habari ambazo hazijathibitishwa   Jammeh amekwenda  uhamishoni nchini Equatorial Guinea na kutamatisha kipindi cha  miaka 22 mamlakani.Awali Jammeh alikubali kushindwa kwenye uchaguzi wa urais uliofanywa mapema mwezi disemba ,lakini akabadili  msimamo na kusisitiza kuwa ulikumbwa na udanganyifu.Hatimaye alisalimu amri baada ya  viongozi wa kanda hiyo kutishia kumng’oa  mamlakani kwa  nguvu. Rais Barrow yungali katika nchi jirani ya Senegal ambako alilishwa kiapo cha kuchukua uongozi wa Gambia  na haijulikani atarejea lini nyumbani.Hata hivyo  kikosi cha muungano cha wanajeshi kutoka kanda hiyo kilikaribishwa kwa vifijo na nderemo kilipowasili katika mji mkuu wa nchi hiyo Banjul kuandaa makaribisho ya rais Barrow.Maelfu ya raia walikusanyika nje ya ikulu ,kuwakaribisha wanajeshi hao ambao walipatiwa jukumu la kuhakikisha usalama kwenye jengo hilo.