Msako wa kuwaokoa walimu waliotekwa nyara Garissa umeanza

Maafisa wa usalama wameanzisha msako mkali katika kaunti ya Garissa na kwenye eneo la mpaka wa Somalia kuwaokoa walimu wawili waliotekwa nyara kutoka kambi ya wakimbizi ya Hagadera hapo jana. Inadaiwa majangili waliojihami walivamia shule za msingi na upili za Al-Huda usiku wa kuamkia leo na kufyatua risasi kiholela. Wakazi wanasema majangili hao walioonekana kufahamu vyema shule hizo waliwalazimisha walimu kufungua milango ya nyumba zao kabla ya kuwateka nyara walimu watatu wa kiume ambao si wenyeji wa eneo hilo. Mmoja wa walimu hao hata hivyo alifaulu kutoroka. Kwenye maungumzo kwa njia yaA�simu, mrakibu wa eneo la Kaskazini Mashariki Mohamud Saleh alipuzilia mbali dhana kuwa shambulizi hilo lilitekelezwa na wanamgambo wa kundi la al Shabaab akisema msako dhidi ya wavamizi hao unaendelea. Alisema maeneo ya Amuma, Abdi Sugow, Alinjugur, Kulan na Liboi kwenye mpaka kati ya Kenya na Somalia yamefungwa ili kuhakikisha majangili hao hawatorokei nchini Somalia. Alisema maafisa wa usalama wanawasiliana na wenzao nchini Somalia katika juhudi za kuwaokoa walimu hao. Kufuatia kisa hicho, shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi limesitisha shughuli zake katika kambi hiyo ya wakimbizi isipokuwa utoaji msaada wa chakula.