Moto mkubwa wateketeza kituo cha central police jijini Nairobi

Moto mkubwa ulizuka leo asubuhi katika nyumba za polisi katika kituo cha Central jijini Nairobi na kuteketeza baadhi ya nyumba hizo. Milipuko inayoshukiwa kuwa ya mitungi ya gesi ilisikika huku wazima moto wakijizatiti kuuzima moto huo unaodaiwa ulisababishwa na hitilafu ya umeme. Moshi uliofuka ulitanda hadi katika seli za kituo hicho cha polisi na majengo mengine na hata barabarani. Polisi walifunga barabara ya University Way kuwaruhusu wazima moja wa kaunti ya Nairobi kuzima moto huo, hali iliyosababisha msongamano mkubwa wa magari. Polisi wamesema hakuna visa vya majeruhi vilivyoripotiwa lakini uchunguzi unafanywa kuhusu kisa hicho.