Mmoja auawa na wawili kujeruhiwa kufuatia maandamano dhidi ya utawala wa Rais Joseph Kabila ya Jamuhuri ya demokrasia ya Kongo

Mtu mmoja aliuawa na wengine wawili kujeruhiwa katika jamhuri ya demokrasia ya Kongo kufuatia mtafaruku kati ya maafisa wa usalama na waandamanaji waliokuwa wakielekea mjini Kinshasa kushinikiza kujiuzulu kwa rais Joseph Kabila. Maandamano hayo yalioandaliwa na kanisa Katoliki yalianza baada ya misa ya jumapili lakini polisi walizingira makanisa na kufunga barabara. Inasemekana kuwa mwana-harakati mmoja aliuawa kwa kupigwa risasi nje ya kanisa la mtakatifu Benoit wakati polisi walikuwa wakiwatawanya waandamanaji. Kanisa katoliki limeandaa msururu wa maandamano tangu mwishoni mwa mwaka uliopita baada ya kutibuka kwa uchaguzi mkuu wa mwaka-2016. Rais Kabila alikuwa ameahidi kuandaa uchaguzi wa uchaguzi na bunge mwaka jana lakini akaahirisha uchaguzi huo hadi mwishoni mwa mwaka huu. Hata hivyo maafisa wa tume ya uchaguzi wamesema uchaguzi huo huenda usiandaliwe jinsi ilivyopangwa kutokana na matatizo ya kifedha na kiufundi, jambo ambalo limewakera zaidi raia wa nchi hiyo.