Mlipuko Nchini Uturuki Yaua Watu 28

Mlipuko mkubwa umetokea katika mji mkuu wa Uturuki Ankara na kusababisha vifo vya watu 28 na kuwajeruhi wengine 61.

Kwa mujibu wa maafisa nchini humo, gari lililokuwa limejaa vilipuzi linasemekana kuvilipua karibu na majengo ya bunge la taifa hilo na makao makuu ya kijeshi.

Naibu waziri mkuu wa Uturuki Bekir Bozdag alilitaja shambulizi hilo kuwa kitendo cha ugaidi. Hakuna kundi lolote ambalo limedai kuhusika na shambulizi hilo. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa baadaye, rais wa taifa hilo Recep Tayyip Erdogan amesema kuwa uturuki iko tayari kujitetea na kujikinga dhidi ya mashambulizi yote ndani na katika mipaka yake.

Erdogan ameahirisha ziara aliyokuwa akitarajiwa kufanya nchini Azerbaijan hivi leo. Aidha waziri mkuu Ahmet Davutoglu pia ameahirisha ziara yake aliyotarajiwa kufanya jijini Brussels Ubelgiji. Marekani imeshtumu vikali shambulizi hilo.