Mlinzi wa Moses Wetangula Simon Lonyang afikishwa mahakamani

Mlinzi wa kibinafsi wa seneta mteule wa Bungoma Moses Wetangula alifikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kuzua vurugu na kuzuia kukamatwa hali ambayo ni kinyume cha sheria. Simon Lonyang anayedaiwa kuingia kwa nguvu kwenye mahakama ya juu akiwa na bunduki alikanusha mashtaka hayo na kuachiliwa A�kwa dhamana ya shilingi elfu-20 na kuagizwa kuacha kitambulisho chake cha kitaifa mahakamani kusubiri kusikizwa kwa swala hilo tarehe 18 mwezi ujao. Lonyang ambaye amefutwa kazi kwenye huduma ya taifa ya polisi kufuatia vurugu hiyo alifikishwa mbele ya hakimu mkuu Francis Andayi na kushtakiwa kwa kuzua vurugu, kumzuia afisa wa polisi kufanya kazi yake na kuingia kwa nguvu kwenye mahakama ya juu akiwa na bunduki. Lonyang ambaye alikamatwa siku moja baada ya tukio hilo na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Central alikanusha mashtaka hayo. Seneta mteule wa Bungoma Moses Wetangula amesema atapambana kisheria dhidi ya kuachishwa kazi kwa mlinzi wake. Kwingineko afisa mkuu wa maswala ya kifedha katika kaunti ya Nairobi Luke Gatimu na maafisa wengine sita wakuu waliokamatwa siku ya Jumatatu kuhusiana na madai ya matumizi mabaya ya mamlaka huenda wakazuiliwa kwa siku saba baada ya upande wa mashtaka kuomba muda zaidi kukamilisha uchunguzi wao. Maafisa hao ambao wamehojiwa na idara ya upelelezi wameripotiwa kupatikana na shilingi milioni saba pesa taslimu katika ukumbi wa City Hall jijini Nairobi na gavana Mike Sonko aliyefanya ziara ya ghafla kwenye afisi yao.