Mkutano Wa Maombi Wa CORD Uliosubiriwa Kwa Hamu Machakos Wakosa Kufanyika

Mkutano wa maombi wa muungano wa Cord uliosubiriwa kwa hamu mjini Machakos uliopangiwa kuandaliwa jana haukufanyika baada ya muungano huo kuuahirisha hadi juma lijalo ili kuwawezesha wabunge waliokuwa wamekamatwa na kushtakiwa mahakamani kuhusiana na matamshi ya chuki kupumzika. Muungano huo ulisema kuwa utatoa habari zaidi hii leo kuhusiana na maandamano yao ya kila wiki. Wapinzani hao walisema kuwa maandamano hayo yatasalia kuahirishwa kuwezesha mashauriano yanayoendelea kuhusu mzozo juu ya tume ya IEBC. Muungano wa Cord ulikuwa umepanga kuandaa mkutano wa maombi hapo jana kukabiliana na kile wanachokitaja kuwa kukandamizwa kwa uhuru wa kujieleza kufuatia kuzuiliwa kwa wabunge wanane kuhusiana na madai ya uenezaji matamshi ya chuki. Hata hivyo wabunge hao waliachiliwa kwa dhamana. Mnamo siku ya Ijumaa gavana wa Machakos, Dr. Alfred Mutua, alikubali kuandaliwa kwa mkutano huo lakini akawaonya waandalizi kujiepusha na vitendo vyovyote vya ghasia wakati wa mkutano huo wa maombi.