IEBC Wafanya Mkutano Na Kamati serikalini Kuhusu Malipo Yao

Makamishna wa tume huru ya uchaguzi na mipaka wanakutana na kamati ya wadau mbalimbali serikalini kwa mashauriano kuhusu utaratibu wa kuwalipa mafao yao. Kamati hiyo inajumuisha wadau kutoka wizara ya fedha, afisi ya mwanasheria mkuu, wizara ya usalama wa kitaifa, wizara ya utumishi wa umma na tume ya kuwianisha mishahara na marupurupu ya watumishi wa umma. Kulingana na taarifa ya hatibu wa serikali Eric Kiraithe, kikao cha kwanza kitajadili kiasi cha mafao ya makamishna hao kabla ya kuondoka afisini. Kiraithe alisema majadiliano hayo yatajikita katika sheria na kwamba serikali inatambua kuwa sheria ya marekebisho ya mfumo wa uchaguzi itaanza kutekelezwa tarehe 4 mwezi ujao. Makamishna wa tume ya IEBC wanatarajiwa kuondoka afisini kufuatia shinikizo za upinzani ambao ulidai hawangeweza kusimamia uchaguzi huru na wa haki. Walishutumu tume hiyo kwa kuegemea upande wa serikali, madai ambayo makamishna hao yamekanusha vikali.