Mipango ya kumshitaki rais Mugabe yaanzishwa

Kiongozi wa chama cha vigogo wa vita vya ukombozi nchini Zimbabwe, amesema kuna mipango ya kumshitaki rais Robert Mugabe jinsi ilivyoazimiwa  baada ya kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 93 kukataa kung’atuka mamlakani kwenye hotuba mubashara kwa taifa jana  usiku.  Chris Mutsvangwa ambaye alikuwa akiongoza harakati za kumuengua Mugabe mamlakani,aliliarifu shirika la habari la REUTERS kuwa huenda hatua hiyo ikatekelezwa baada ya Mugabe kukataa kujiuzulu. Awali kwenye mkutano uliofanywa mjini Harare,chama tawala cha ZANU-PF kilimwondoa rais Mugabe na wapambe wake kwenye uongozi wa  chama na kimempa muda wa saa 24 kujiuzulu la sivyo kitawasilisha mashtaka. Ushawishi wa Mugabe,mwenye umri wa miaka 93 umepungua sana tangu  alipong’olewa mamlakani siku ya jumatano wiki iliopita. Rais Mugabe aliwakera raia na viongozi wa majeshi ya nchi hiyo alipomtimua uongozini naibu wake Emmerson Mnangagwa. Kiongozi huyo wa Zimbabwe alishutumiwa kwa kubuni mbinu za kumweka mkewe kuwa naibu wa rais. Shinikizo za raia  za kumtaka Mugabe ajiuzulu zimeongezeka tangu wiki jana,huku wakitaka kufanywe mabadiliko ili kurejesha hali ya kawaida katika taifa hilo.