Miili ya wawili yapatikana imetupwa Mombasa

Miili ya Mwanaume na mwanamke wa umri wa kati ya miaka 60 na 70 ilipatikana imetupwa kwenye barabara moja ya sehemu ya vijijini katika jiji la pwani la Mombasa. Afisa mkuu wa polisi katika sehemu hiyo Christopher Rotich alisema uraia wao haujulikani kwa sababu hawakupatikana na stakabadhi zozote. Miili hiyo ilipatikana imefungwa kwenye blanketi na kuachwa kando ya klabu kimoja cha usiku nje ya jiji la Mombasa. Chama cha wenye hoteli na huduma za kitalii kilisema kilichunguza katika hoteli za eneo hilo la pwani na hakuna hoteli iliyoripoti kupotea kwa wageni wake.