Miguna Miguna akataa kujibu mashtaka katika mahakama ya Kajiado

Miguna Miguna aliyejitangaza kuwa jenerali wa vuguvugu haramu la NRM amekataa kujibu mashtaka dhidi yake katika mahakama moja ya Kajiado akisema jaji Luka Kimaru anamsubiri katika mahakama kuu ya Milimani jijini Nairobi. Miguna alifikishwa katika mahakama hiyo ya Kajiado licha ya jaji Kimaru kuagizwa jana awasilishwe katika mahakama ya Milimani leo asubuhi..Awali afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma ilieleza mahakama jijini Nairobi kuwa Miguna Miguna alishtakiwa leo asubuhi katika mahakama moja ya Kajiado. Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyowasilishwa mahakamani, Miguna alishtakiwa kwa kuhudhuria na kushiriki katika uapisho wa kusaliti taifa. Vile vile alishtakiwa kwa kuwa mwanachama wa kundi haramu la NRM na kuandaa mkutano haramu katika bustani ya Uhuru jijini Nairobi ambapo uapisho huo ulifanyika tarehe 30 mwezi Januari. Akidai kuwa hati hiyo ya mashtaka ina kasoro na haiaminiki, mawakili wa Miguna wanataka mahakama kuu ya Milimani kuagizaA� mahakama ya Kajiado kumwachilia huru mteja wao na kuwasilisha faili ya mashtaka katika mahakama ya Milimani jijini Nairobi.