Michael Joseph Ateuliwa Kuwa Mwenyekiti Wa KQ

Aliyekuwa afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya mawasiliano ya Safaricom, Michael Joseph ameteuliwa kuwa kaimu mwenyeiti wa bodi ya shirika la ndege la Kenya Airways kuchukua mahali pa Dennis Awori. Uteuzi wake unafuatia mzozo uliokumba shirika hilo huku marubani wakitishia kugoma wakiwataka Awori, afisa mkuu mtendaji wa kampuni hiyo Mbuvi Ngunze na maafisa wa ngazi za juu kujiuzulu. Marubani hao wanawalaumu maafisa hao kwa usimamizi mbaya ambao umelisababishia shirika hilo hasara kubwa. Kufuatia hatua hiyo, marubani hao wameahirisha mgomo wao uliopangwa kuanza leo. Masaibu ya shirika hilo yalianza juma lililopita wakati wahudumu wa ndege wa muda 700 na maafisa wa uhusiano mwema walipogoma kulalamikia kile walichotaja kuwa mishahara finyu. Wahudumu hao waliokodishwa kutoka kampuni ya Career Directions walikuwa wamekaidi kurejea kazini hadi pale malalamishi yao yatakaposhughulikiwa, hali iliyosababisha kuchelewa kwa safari za ndege za shirika hilo Jumapili. Waziri wa leba Phyllis Kandie hapo jana aliandaa mkutano na wasimamizi wa shirika la ndege la Kenya Airways na waakilishi wa chama cha marubani hapa nchini katika juhudi za kukomesha mzozo huo.A�