Mgawanyiko waibuka miongoni mwa waislamu kuhusu Eid ul Adhah

Mgawanyiko uliibuka jana miongoni mwa waumini wa dini ya kiislamu hapa nchini wakati wa sherehe ya Eid ul Adhah huku waumini hao wakikaidi ushauri wa kadhi mkuu Ahmed Muhdhar wa kuadhimisha sikukuu hiyo leo. Hii ni baada ya waumini hao kutatizika kuhusu ikiwa sherehe ya Eid ul Adhah inafaa kuandaliwa jana au leo.

Waziri wa utalii, Najib Balala ameahidi kuongoza juhudi za kufungua afisi ya dini ya kiislamu hapa nchini. Akiongea jana katika kituo cha Sheikh Zayed huko Mombasa alipohudhuria maombi maalum ya Idd-ul-Adha, Balala alisema jamii ya waislamu imekosa kuungana na kuwa na msimamo mmoja kuhusu tarehe za mafungo ya mwezi mtukufu wa Ramadhan na wakati wa kuandaliwa kwa sherejhe mbili muhimu za kiislamu.

Kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Aden Duale anataka tume ya kuajiri wafanyikazi wa idara ya mahakama imchukulie hatua kadhi mkuu sheikh Ahmed Modhar kwa madai ya kuwapotosha waislamu kuhusu siku ya kuandaliwa kwa sherehe ya Eid ul Adhah. Akiongea alipoungana na waumini wa kiislamu katika kuadhimisha siku kuu hiyo katika uwanja wa General Muhamud huko Garissa, Duale aliwataka wasomi na wadau wengine wa dini ya kiislamu wakutane kujadilia mienendo ya kadhi mkuu.