Mexico Yakashifu Pendekezo La Marekani La Kutoza Ushuru Bidhaa Zake.

Mexico imekashifu pendekezo la Marekani la kutoza ushuru wa asilimia 20 bidhaa kutoka nchi hiyo kugharamia ujenzi wa ukuta kati ya nchi hizo mbili. Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Mexico, Luis Videgaray alisema ushuru huo utasababisha ongezeko la bei ya bidhaa kutoka nchi hiyo zinazouzwa nchini Marekani. Awali rais wa Mexico alikuwa amefutilia mbali ziara yake nchini Marekani kutokana na utata kuhusu ujenzi wa ukuta huo. Rais Donald Trump aliahidi kujenga ukuta huo wakati wa kampeni zake za urais mwaka jana. Mapema wiki hii, rais Trump alitia saini agizo la kujenga ukuta huo wa umbali wa kilomita 3,200 kwenye mpaka kati ya nchi hizo mbili. Akiongea jana, Videgaray alisema ushuru huo utakaotozwaA� bidhaa za Mexico zinazoingizwa nchini Marekani hautaifanya nchi yake kugharamia ujenzi wa ukuta huo lakini ni njia ya kuwafanya raia wa Marekani kulipia mradi huo kupitia ununuzi wa bidhaa za Mexico kwa bei ya juu. Mexico huuza bidhaa za thamani ya dola bilioni 300 nchini Marekani kila mwaka.