Mawakili wa Waiguru waitaka EACC kutoa taarifa iliyowasilishwa na Kabura

Kundi la mawakili wa gavana wa kaunti ya Kirinyaga Anne Waiguru linaitaka tume ya maadili na kupambana na ufisadi-EACC kuwasilisha matokeo ya uchunguzi wake kuhusu taarifa ya kiapo iliyowasilishwa na Josphine Kabura ambaye alikuwa mshukiwa mkuu kwenye ile kashfa ya kwanza ya shirika la huduma ya vijana kwa taifa- NYS.

Kwenye barua iliyoandikwa tarehe 23 mwezi huu Waiguru anasema kuchelewa kwa tume ya EACC kuwasilisha matokeo ya uchunguzi wake kunaendelea kumharibia sifa akitaja ripoti ya hivi majuzi kuhusu ufisadi ya kampuni ya IPSOS. Kwenye barua iliyoandaikiwa afisa mkuu wa tume ya EACC, Halaqhe Waqo, Waiguru anasema ameandikia tume ya EACC barua mara kadhaa lakini inasikitisha kwamba miaka miwili na nusu baadaye tume hiyo haijajibu ombi lake.

Mawakili wa kampuni ya Issa and Company sasa wanataka kutolewa mara moja matokeo ya taarifa ya kiapo ya Bi. Kabura na faili hiyo kuwasilishwa kwa ofisi ya mkurugenzi wa mashataka ya umma. Mwezi Februari mwaka wa 2016, Bi. Kabura aliwasilisha taarifa ya kiapo akimlaumu Bi. Waiguru na maafisa wengine wakuu serikalini kwa kupanga njama ya kuiba shilingi milioni 791 kutoka shirika la NYS kupitia utoaji zabuni za kushukiwa.

Hatua hii ilisababisha tume ya EACC kuwaagiza Waiguru na maafisa wengine waliotajwa kwenye taarifa hiyo kuandikisha taarifa zao. Bi Waiguru baadaye aliondolewa lawama kwenye kashfa ya hiyo ya kwanza iliyokumba shirika la NYS ambapo tume ya EACC ilimuandikia barua mkuu wa utumishi wa umma Joseph Kinyua kumfahamisha kwamba haikupata ushahidi wa kutosha ili kuweza kumfunguilia mashtaka Waiguru.