Mawakili wa Uhuru wasema kesi ya NASA haina msingi

Kundi la mawakili wa Rais Uhuru Kenyatta wakiongozwa na Fred Ngatia, jana lilikosoa kesi iliyowasilishwa mahakamani na Raila Odinga kupinga uchaguzi wa urais, wakisema haina msingi. Katika taarifa yake kwa mahakama ya juu, Ngatia alitoa wito wa kufutiliwa mbali kwa kesi hiyo kwani rais Uhuru Kenyatta alipata zaidi ya asilimia 25 ya kura katika kaunti 39 kama inavyohitajika kisheria. Aidha alisema wagombezi wote wa urais walikuwa na maajenti katika vituo vyote vya kupigia kura hapa nchini, waliotia saini fomu zinazotangaza matokeo ya urais. Ngatia pia alisema vituo 11,155 vya kupiga kura ambavyo havikuwa na mitandao ya 3G na 4G, havikuathiri wapigaji kura milioni 3.4 waliosajiliwa katika sehemu husika.A�

Awali, wakili mkuu Ahmednasir Abdulahi alipuuzilia mbali kesi hiyo akisema haijaafiki kiwango kinachohitajika, akiitaja kuwa uvumi. Abdullahi alisema mwasilishi wa kesi hiyo alitilia maanani matokeo, na kukosa kuiambia mahakama namna ambayo watu milioni 14 walipiga kura katika uchaguzi huo wa tarehe 8 mwezi Agosti.