Matuta kwenye barabara kuu ya Thika Superhighway yaanza kuondolewa

Halmashauri ya kitaifa ya barabara kuu imeanza kuondoa matuta kwenye barabara kuu ya Thika Superhighway kufuatia shinikizo za gavana wa kaunti ya Nairobi, Mike Sonko. Mwezi Februari, mahakama kuu iliagiza halmashauri hiyo kuondoa matuta hayo kwenye maeneo ya Survey of Kenya, Homeland na Kenya Breweries na kujenga daraja. Haya yalifuatia kesi iliyowasilishwa na Sonko mwezi Aprili akipinga uamuzi wa aliyekuwa gavana wa kaunti ya Nairobi Evans Kidero wa kufanyia marekebisho barabara za jiji la Nairobi kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari. Kwenye taarifa, halmashauri hiyo ilisema inajizatiti kulainisha shughuli za uchukuzi kwenye barabara hiyo kwa manufaa ya waendeshaji magari na wale wanaotembea kwa miguu.